Monday 7 September 2015

Binti aeleza jinsi mzimu wa babu unavyomdai hirizi aliyopoteza!


binti huyu hakuwa muongeaji. Hii ilimtatiza sana mama yangu ambaye ni mchangamfu na hupenda mazungumzo. Mama ambaye amekuwa akishinda naye ninapokuwa kazini, ndiye aliyeshuhudia vituko vingi zaidi.

Kwa mfano, hata kama wamekaa wote eneo moja, binti huyu lazima ampige mama kisogo au achukue mkeka na kwenda kulala mbali na alipo mama.

Au anaweza kuvua ndala na kwenda nyuma ya nyumba kwenda kufanya mambo yake. Siku moja alifanya hivyo, kidogo mama akasikia mtu anatikisa bomba za maji ambazo zimewekwa nyuma ya nyumba. Ni mfano wa mtu anapigana na kitu kwani alikuwa akitoa sauti kubwa.

Ilibidi mama anyanyuke na kuingia ndani kwenda moja kwa moja chumbani kwake ambako ni usawa wa dirisha anakotikisa bomba Yule binti. Hizi ni bomba za maji zilizofungwa na kuegemezwa ukutani nyuma ya nyumba.

Mama kuchungulia akamuona binti anazipiga zile bomba huku akitamka “nitarudi…nitarudi msiniumize…nitarudi”.


Mama kuona jinsi anavyotumia nguvu nyingi kupigana na bomba zile akamsemesha. Ghafla akashtuka, akaondoka haraka mahali pale.

Baadaye mama alipomuuliza alikuwa anaongea na nani akajibu mzimu wa babu yake, ukimtaka arudi nyumbani kwa kuwa hapo alipo hana ulinzi baada ya kupoteza hirizi aliyopewa na mama yake kabla ya kuja Dar.

Binti huyu alisema wakati anatoka  Mwanza kuja Tabora, kisha Dar, begi la nguo lilishushwa njiani maeneo ya Shinyanga na ndani mlikuwa na nguo nyingi, pia hirizi aliyopewa na mama yake. Hii anadai n kinga (Ulinzi) aliyoagiza babu yake(marehemu) apewe.

Siku nyingine akaanza tabia ya kumwacha mama na kutoka nje ya geti kisha kurejea. Mama akimuuliza ulienda wapi anamjibu ni kuona kama anaweza kuwaona watu wa nyumbani kwao.

Mama aliponijulisha hilo, nikawa nafunga huo mlango wa geti na kumuachia mama funguo. Alipojaribu akakutwa umefungwa akamwambia mama hata ukifungwa akitaka kuondoka, wala hatatumia mlango, atapaa kiaina. Duh! Ulikuwa mtihani mkubwa sana. Eti atapaa?

Ndipo ikabidi nimdadisi vizuri. Baada ya chai nikamhoji. Mbona kimya sana? Mama akadakiza, anataka kuondoka, amepoteza vitu vyake hasa hirizi. Nikashtuka. Hirizi? Ilikuwa ya nini?

Nikamuuliza ndipo akatoboa siri. Akasema kuwa hapo alipo yeye ni mzimu wa babu.

Ipo hirizi ilipotea pamoja na begi la nguo wakati anakuja Dar. Sasa babu yake huyo mzaa mama yake ambaye ni marehemu, amekuwa anamtokea hadharani au usingizini akimuuliza hirizi iko wapi.

Yeye humjibu imepotea. Akasema “Ananijia mchana ananiambia hirizi iko wapi, namjibu imepotea. Ananiambia basi ondoka hapo hapafai unaharibu kazi zetu.”

Nikamuuliza; anapokujia amevaa nini? Akajibu  kanzu. Akaongeza “hata mama yangu hunitokea mchana kweupe akiniuliza zile nguo ziko wapi, namjibu zimepotea. Ananiambia basi rudi nyumbani huwezi kukaa hapo kazi zetu zinaharibika”.

Nilipomwambia mlinzi mkuu ni Mungu pekee na siyo hirizi za wanadamu, binti akatiririsha machozi. Nikamuuliza kama aliwahi kwenda kanisani akajibu ndiyo wakati akiwa na baba yake, lakini baada ya kwenda kwa mama akakatazwa.

Mpenzi msomaji wangu, baada ya maelezo hayo ya binti, nikaanza sasa kupata picha kwanini binti yule hakuwa wa kawaida. Nimekaa na mabinti wa kazi  mbalimbali lakini huyu vituko vyake vilikuwa kiboko.

Lakini kwa kuwa namtumainia Mungu wangu kwa kila jambo, sikuwa na hofu yoyote naye. Ni kwa sababu nilimwachia Mungu ashughulike na tatizo hilo. Maana amesema, “Nitawapigania ninyi, nanyi mtakaa kimya”. Kutoka 14:14.

 Hivyo ndio vituko vya binti huyo ambaye baada ya kuona vituko vinazidi huku akiwa hana raha nikamwita jamaa yake aliyemleta, akamwambia sababu za kutaka kuondoka akisema wazi juu ya hirizi na mzimu wa babu, nikatoa nauli akamsafirisha kwao.
Ama kweli Maisha Ndivyo Yalivyo.

chanzo:NIPASHE

No comments:

Post a Comment