Monday 14 April 2014

Ufuska waigeuza Dar `Sodoma` -2,Mkuu wa wilaya aangua kilio.

Vitendo vya ufuska vinavyoendelea katika eneo lililopo Mbagala Zakhem katika manispaa ya Temeke, ambalo ni maarufu kwa kuwavutia wanawake wengi na wanaume wanaojihusisha na biashara hiyo haramu, vimekuwa tishio siyo tu kwa mazingira, bali pia maambukizi ya ukimwi na athari za madawa ya kulevya. 

Kinachosikitisha zaidi ni kuwa jeshi la polisi wilayani humo linajua yanayofanyika eneo hilo lakino hakuna hatua madhubuti ambazo zimechukuliwa kudhibiti vitendo hivyo haramu ambavyo pamoja na kutishia afya ya binadamu, pia inachafua taswira ya taifa letu ndani na nje ya nchi.


Isitoshe, hata viongozi wengine akiwamo mkuu wa wilaya ya Temeke, Siphia Mjema, inaonekana kushtushwa na taarifa za kuwapo kwa ufuska huo kiasi cha kudondosha machozi kwa kutoamini kwamba hali hiyo ipo katika eneo analosimamia kiutawala

UKIMWI NA DAWA ZA KULEVYA
Pamoja na kuwapo taarifa ya matumizi ya kondomu nyingi katika eneo hilo, miongoni mwa wanawake wanalalamikia vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wateja wao kuzipasua wakati wa kujamiiana.

Msichana mwenye umri wa miaka 20 (jina linahifadhiwa), anayejihusisha na biashara hiyo, anasema kupasuliwa kwa kondomu ni jambo la kawaida kuwatokea, na kwamba inapokuwa hivyo, wanashirikiana kumtoza mteja mhusika faini ya Shilingi 15,000.

Anasema vitendo hivyo vinahatarisha afya yao na kuwaweka katika hatari ya kuambukizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Pia msichana huyo anaitaja athari nyingine kuwa ni kondomu kupenya hadi sehemu ya siri, hivyo kusababisha kufanyiwa upasuaji.

"Pamoja na kukumbana na hatari hizo, hatuna la kufanya kwa sababu sisi tunatafuta pesa kwa ajili ya kuhudumia familia zetu," anasema.

Wanakitaja kituo cha afya cha Zakhem kuwa eneo muhimu kwao kwa ajili ya upasuaji wa kuondolewa kondomu zinazonasa, huku wakitozwa fedha nyingi.

Pamoja na hayo, ilibainika kuwa sehemu kubwa ya wahusika wa biashara hiyo ni watumiaji wa dawa za kulevya.

MKUU WA WILAYA AANGUA KILIO
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema, alipofuatwa ofisini kwake na kuelezwa uwapo wa soko hilo, aliangua kilio.

Mjema alijikuta akilia baada ya kutoamini taarifa aliyotakiwa kuitolea ufafanuzi, akisema kinaweza kuaminika kwa haraka kama kimeonekana katika picha za mnato na si eneo la utawala wake.

 “Jambo hili limenishtua kiasi kikubwa, ni hali ya unyama unaotendeka, haiwezekani binadamu na akili zao wakafanya vitendo hivyo hadharani," alisema na kuanza kuangua kilio.

Alisema hana taarifa kuhusiana na kuwapo kwa biashara haramu hiyo, hivyo atafuatilia na kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika.

"Kinachoniumiza kuona vijana hawa wanaangamia huku wenyewe wakijiona, ikiwa leo mtoto anahusika na mambo hayo hali ya baadaye itakuwaje, natahakikisha vitendo hivi vinakoma mara moja," anasema.

RPC: NINAFAHAMU, NIMEONA
Hata hivyo, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Engelbert Kiondo, anathibitisha kulifahamu eneo hilo na biashara ya ngono inayofanyika hapo.

Alisema, mkakati wa kuidhibiti biashara haramu hiyo unaandaliwa kwa vile matumizi ya nguvu peke yake hayawezi kuleta suluhu ya kudumu.

"Suala la dadapoa linatakiwa kutumia akili na elimu zaidi, ukitumia nguvu lazima utashindwa kwa sababu sheria ya nchi haielezi chochote," alisema Kiondo.

Hata hivyo alisema anakerwa kwa kile kinachofanyika katika eneo hilo kwani inadhalilisha na kuondoa utu wa mtu.
chanzo:Nipashe

No comments:

Post a Comment